Skip to content
domain-name

Kwa Nini Unahitaji Domain Name?

Kama tulivyoona katika post iliyopita, pasipo domain name ingebidi uandike ip address moja kwa moja katika browser yako ili kufika kwenye website husika.

Hebu fikiria: ilibidi uandike 64.4.11.42 badala ya Microsoft.com! IP address kama hii ni ngumu kuikumbuka, inahitaji utaalamu ili kuielewa maana yake, na pia hata kuiandika.

Pamoja na ukweli huu, zifuatazo ni sababu zinazojibu swali hilo hapo juu – Kwa nini unahitaji domain name? – kwa mapana zaidi:

1. Ni utambulisho wako wa pekee mtandaoni

Hakuna biashara mbili/watu wawili tofauti wanaoweza kuwa na domain name zinazofanana wakati wowote. Hivyo domain name inakutambulisha kipekee mtandaoni.

2. Inatambulisha zaidi jina la biashara yako

Tutaona katika sehemu inayofuata kwamba unapaswa kuchagua domain name inayosadifu jina la biashara yako, ama huduma inazotoa, ama bidhaa inazouza. Kwa hivyo domain name itatoa muhtasari wa biashara yako: ni nini, inatoa nini, inafanya nini, n.k.

3. Inasaidia wateja wako kuikumbuka anwani yako

Domain name ni anwani yako mtandaoni. Mtu anapokuwa mtandaoni, anaitumia kufika kwenye website yako. Na kwa kuwa domain name ni jina linaloeleweka na si namba kama ilivyo IP address, ni rahisi kuikumbuka

4. Inaupa chapa mwonekano wako kama biashara katika soko

Ukiwa na domain name unaweza kuiweka katika business card, vipeperushi, barua, na vifaa vingine unavyotumia kwa ajili ya kuitangaza biashara yako. Pia unaweza kuwa na barua pepe zinazoendana na domain name yako, mfano; jina.lako@domain-name-yako.co.tz

5. Inaongeza uaminifu na weledi kwa biashara yako machoni pa wengine

6. Inalinda jina la biashara yako mtandaoni

Katika sababu ya kwanza tumeona kuwa katika wakati wowote hakuwezi kuwa na domain names mbili zinazofanana.

Tuseme bwana Maganga anafanya biashara ya kuuza mitumba. Na biashara hii ameisajili kwa jina Mitumba kwa kuwa aliona ndio jina linaloeleweka, lenye kuielezea biashara yake kwa urahisi, ufupi, na linaloweza kukumbukwa. Na pia kwa sababu hizo hizo amekusudia kusajili domain name ya mitumba.co.tz kwa ajili ya website yake.

Hata hivyo bwana Mkude amekwishasajili domain name yake kwa jina hilo: mitumba.co.tz! Hii inamaanisha nini? Inamaanisha kuwa japo Mitumba ndio jina la biashara ya bwana Maganga kisheria, lakini hataweza tena kutumia domain name mitumba.co.tz kwa kuwa tu imeshasajiliwa na mtu mwingine.

Kama wewe ni mmoja wa akina bwana Maganga wengi walioko huku mtaani POLE! Lakini pia unaweza kumtafuta bwana Mkude na kujaribu kuongea naye kuona kama anaweza kukuuzia hiyo domain name, ingawa mara nyingi gharama zake huwa ni mara kadhaa ya gharama halisi
za kusajili domain name katika hali ya kawaida.

Unachagua vipi domain name?

Kwa kuwa tumeona domain name ni utambulisho wako/wa biashara yako mtandaoni, haitarajiwi ukurupuke katika kuichagua. Na nimeona nikupe miongozo kadhaa ya kufuata katika mchakato wa kuichagua. Hebu tuanze kuiangalia:

 • Iwe fupi kadiri inavyowezekana
 • Iwe rahisi kukumbuka
 • Iwe rahisi kutamka
 • Ihusiane moja kwa moja ama na jina la biashara yako, au maneno yanayotumika katika nyanja husika ya biashara yako, au yaliyomo katika website yako – bidhaa/huduma/mafundisho
 • Isiwe inayoeleweka kwa maana zaidi ya moja
 • Isitumie vifupisho
 • Angalia mkakati wako wa masoko

Miongozo hii saba inatosha kukusaidia kuchagua domain name itakayoipa biashara yako utambulisho wa pekee na unaolipa mtandaoni. Kwa hiyo kama hauna muda wa kusoma zaidi sehemu hii inaishia hapa, twende sehemu inayofuata: ‘Unasajili vipi domain name’ hapo chini. Vinginevyo kama unataka kujua zaidi, yapo ya kujua zaidi…

Jua zaidi juu ya kuchagua domain name

Kwa biashara, kuwa na domain name ni mkakati mwingine wa kulifikia soko, kujitangaza. Na mkakati huu kama mingine ya kimasoko una lengo la kufanya jina la biashara, ama bidhaa, ama huduma zako kuwa mdomoni ama kichwani mwa wateja wako wa sasa ama wateja watarajiwa. Na utaona miongozo yote hapo juu inakusaidia kufikia lengo hilo! Hebu basi tuiangalie kwa mtazamo mwingine kidogo:

Mkakati wa kimasoko

Bwana Massawe anatoa huduma za utengenezaji wa website. Amekusudia kulifikia soko lake kupitia mtandao pekee. Kwa hivyo analipia matangazo Google, Facebook, YahooZoomTanzania, na kila mahali ambapo anahisi wateja wake wapo.

Na wateja wake wanapokutana na tangazo la biashara yake, wanachofanya ni kubofya tu, na hatimaye kupelekwa kwenye website/facebook page ya biashara yake. Wateja hawa mara nyingi hata hawajui domain name ya biashara ya bwana Massawe; na kwa mkakati wake huu ni kwamba hawahitaji sana kuijua.

Hivyo bwana Massawe anaweza asifuate mwongozo mwingine wowote isipokuwa ule wa mwisho, na akawa na mafanikio aliyoyakusudia
katika soko kwa sababu ya mkakati wake huo wa kimasoko.

Hebu tumuangalie na mama Rutashobya…
Yeye anafanya biashara ya utoaji wa huduma za upishi katika sherehe, misiba na matukio mbalimbali.

Anatarajia watu wataijua biashara yake kupitia bango aliloweka katika mgahawa wake, maandishi yaliyoko ubavuni mwa gari lake analotumia kubebea vyakula, business cards zake na ushuhuda wa wale aliowahi kuwapa huduma zake.

Pia, biashara ikichanganya, amekusudia kulipia matangazo redioni na katika televisheni.

Kwa mkakati huu mama Rutashobya atahitaji kufuata miongozo yote sita iliyopo hapo juu katika kuchagua domain name ili kufikia wateja wake kama alivyokusudia. Kwa nini? Kwa kuwa ni lazima domain name yake iwawezeshe watu kuikumbuka biashara yake.

Jina la biashara VS Maneno

Ni vizuri kujaribu kuchagua domain name yenye jina la biashara/kampuni yako. Na kama unaweza kuweka pia jina la nyanja ya biashara yako bila kwenda kinyume na miongozo hiyo hapo juu, ni vizuri zaidi.

Mfano, jina la biashara yetu ni FanyaICT Solutions, domain name yetu ni fanyaict.net: Kwanza tulihakikisha ndani ya jina la biashara yetu kuna nyanja tuliyomo (ICT). Hivyo ilipokuja suala la domain name hakukuwa na shida sana katika uchaguzi.

Pia unaweza kuongeza mahali biashara yako ilipo badala ya nyanja kama ilivyo kwa zoomtanzania.com.

Chaguo jingine ni kutumia maneno yanayoelezea kile biashara inachofanya badala ya jina la biashara husika. Domain name za maneno zinafaa sana hasa pale ambapo jina la biashara ni refu ama ni gumu kutamka.

Kwa mfano, biashara ya mama Rutashobya hapo juu inayoitwa ‘Mama Rutashobya Catering Services’ inaweza kuwa na domain name ya TunapikaChakula.com. Kama unavyoona domain name hii ni rahisi kukumbuka na pia kutamka.

Maana zaidi ya moja

Domain name ya website ya biashara ya bwana Makame ni 112.com. Miezi mitatu iliyopita, bwana Makame alipata nafasi ya kutoa mada katika siku ya mwisho ya kongamano la wajasiriamali wa Tanzania lililoandaliwa na taasisi moja ya kifedha.

Nafasi hii ilikuwa pia ni fursa ya kuitangaza biashara yake, hasa ukizingatia kuwa wengi wa wajasiriamali waliokuwepo wangeweza kuhitaji huduma zake na hivyo kuwa wateja wake.

Baada ya kumaliza kutoa mada hiyo iliyoonekana kufurahiwa sana na wasikilizaji wake, bwana Makame alihitimisha kwa kusema,”Nakala ya mada hii nimeiweka kwenye website yangu inayoitwa 112.com, hivyo kwa yoyote ambaye angependa kuirejea anaweza kwenda kui-download hapo.”

Zaidi ya nusu ya washiriki wakajikuta wakisema, “Tunaomba urudie jina la website.” Bwana Makame ili kuweka msisitizo akarudia kwa kiingereza, “112.com”. Na wakati anarudia kutaja jina la website yake, washiriki wote walikuwa wameinamia meza zao wakiliandika katika karatasi za madaftari yao. Bwana Makame akatabasamu huku akijisemea moyoni, “angalau watu mia zaidi wataitembelea website yangu na ku-download nakala ya mada hii.”

Miezi mitatu imepita sasa na nakala ya mada ile haijapakuliwa(download-pakua) hata mara moja. Bwana Makame haelewi ni kwa nini, yamkini hata wewe hauelewi ni kwa nini!

Kama kuna mtu angepata nafasi ya kupitia madaftari ya wale washiriki kuona ni nini walichoandika siku ile, bila shaka asingekosa kukuta: mojamojambili.com, 11.com, oneonetwo.com, na yamkini 112.com!

Hawa washiriki kwa jinsi walivyokuwa wameifurahia mada, yamkini mara tu baada ya kongamano walijaribu kuitafuta 112.com bila mafanikio. Nafikiri sasa unajua kwa nini : Domain name ilikuwa na MAANA ZAIDI YA MOJA!

Na vifupisho je?

Domain name za vifupisho si nzuri kutumia. Kama tulivyokwishaona kuwa na domain name pamoja na mambo mengine kuna lengo la kufanya jina la biashara, ama bidhaa, ama huduma zako kuwa mdomoni ama kichwani mwa wateja wako wa sasa ama wateja watarajiwa.

Vifupisho havisaidii kwa namna yoyote kutimiza hili, na mara nyingi huwa havina maana yoyote kwa mtu anayeviona kwa mara ya kwanza.

Na miongoni mwa vitu vigumu, ni kukumbuka kitu usichojua maana yake. Kwa hiyo jitahidi kwa gharama zote kukwepa kuwa na domain name ambayo ni kifupisho cha maneno/majina mengine.

Unasajili vipi domain name?

Kuna njia tatu za kusajili domain name: unaweza ukaisajili mwenyewe, ukamtumia web host wako ama ukamtumia yule atakayekutengenezea website.

Web Host/Mtengeneza website

Kampuni nyingi zinazotoa huduma za hosting, pia zinatoa huduma za usajili kwa wateja wao. Pia watengeneza website wengi pia hupewa jukumu la usajili wa domain name na hosting na wateja wao.

Ukitaka kuisajili domain name yako kwa kutumia web hosts ama watengeneza website, basi wataisajili kwa kutumia Msajili wao aliyethibitishwa.

Faida ya kutumia moja ya njia hizi ni kuwa hawa watu wameshafanya mchakato huu hapo kabla, kwa hiyo wanajua ni nini cha kufanya, na ni wapi pa kwenda, na hili linaokoa muda.

Kuisajili mwenyewe

Hapo itabidi uchague Msajili. Msajili ni kampuni ya usajili ilyothibitishwa na ICANN (Chombo kinachosimamia majina na namba mtandaoni).

Kuna wasajili wengi mtandaoni siku hizi. Lakini kama unataka pendekezo langu basi nitakuambia ni Aptus Solutions kama unataka domain name inayoishia na .tz, vinginevyo ni Tucows.

Mengineyo

Kupyaisha Usajili

Inabidi kila baada ya muda fulani (mara nyingi ni mwaka) upyaishe usajili wa domain name yako. Usipofanya hivyo na usajili ukaisha muda wake, hiyo domain name haitakuwa tena yako, bali itakuwa ya Msajili, na anaweza kuiuza kwa mtu/watu wengine.

Kuhakikisha hilo halitokei, inabidi kuipyaisha kabla ya muda wake kuisha. Pia inabidi kuhakikisha taarifa zako katika usajili ni sahihi, kwa kuwa ni kwa taarifa hizi Msajili ataweza kuwasiliana na wewe na kukupa taarifa yoyote unayohitaji kuijua juu ya domain name yako.

Gharama

Kwa sasa, Tanzania gharama za usajili zinaanzia shilingi 25,000/=. Na baada ya kila mwaka utahitaji kupyaisha usajili kwa gharama hiyo hiyo.

Kwingineko gharama ziko chini zaidi hadi kufikia $0.99 (kama shilingi 2137/= kwa sasa) kwa usajili na $10.99(kama shilingi 23723/= kwa sasa) kwa kupyaisha usajili kila baada ya mwaka.

Nyongeza

Unaposajili domain name, taarifa zako zinaingia katika rekodi inayoitwa WHOIS record (rekodi ya domain names zilizosajiliwa na taarifa za wamiliki wake). Rekodi hii inaweza ikaonwa na yoyote anayehitaji. Na kwa hiyo taarifa zako pia.

Unaweza ukachagua kuruhusu ionwe ama ukaamua kuficha hizo taarifa zako, chaguo linalohitaji gharama zaidi tofauti na za usajili.

Je, biashara yako tayari ina domain name? Ni sababu zipi ambazo sijazielezea zilikusukuma kuwa nayo? Katika kuipata, ulitumia miongozo ipi ambayo sijaitaja? Na ulitumia Msajili yupi kuisajili? Tushirikishane katika comments hapo chini . . .

domain-names

Ijue Domain Name: Ni nini? Inatumika Wapi? Inahusiana na nini?

Mara nyingi unapokuwa ukihitaji kuwa na website kuna majina ambayo hautakwepa kukutana nayo: domain name, hosting account, bandwidth, n.k.

Na kwa kuwa ni muhimu kujua maana zake na uhusiano wake katika utengenezaji wa website ya biashara yako, wiki hii nimeamua tuyaangalia kwa kuanzia na domain name…

Maana

Ili tuelewe vizuri maana ya domain name, kuna majina mengine ya kiufundi inabidi tuyaelewe. Majina haya yana uhusiano wa moja kwa moja na domain name na jinsi inavyofanya kazi.

IP Address

 Anwani ya kifaa chochote mtandaoni inaitwa IP address(Internet Protocal address).

Ni kwa kutumia anwani hii vifaa vilivyoko mtandaoni huwasiliana. Mfano wa IP address ni 1.160.10.240.

Kama unasoma post hii bila shaka uko mtandaoni, kwa hivyo unaweza kutumia google kujua IP address ya kifaa unachotumia (kompyuta,simu,n.k): andika ‘my IP address’ ama ‘what is my IP address’ na kisha tafuta; google italeta IP address ya kifaa ambacho kimetumika kutuma ombi hilo.

Domain Name

 Domain name ni jina linaloeleweka na linaloweza kukumbukwa kwa urahisi la IP address ya kompyuta zinazohifadhi website mtandaoni. Mfano wa domain name ni kama: fanyaict.net, google.com, ifm.ac.tz, maxima.co.tz, n.k.

Pasipo domain name ingehitaji uandike 74.125.224.72 badala ya google.com!

DNS

Hata hivyo kwa kuwa mtandao umejengwa juu ya IP address na si domain names kuna mfumo wa kutafsiri na kuhusianisha domain name na IP address yake. Mfumo huu unaitwa DNS(Domain Name System). Kila unapoandika domain name, mfumo huu huitafsiri kwenda kwenye IP address yake kabla ya kukuwezesha kufika katika website husika.

URL

URL (Uniform Resource Locator) ni anwani ya maneno ya mtandaoni. Anwani hii inabeba taarifa nyingi kama domain name, jina la ukurasa unaotakiwa, faili ambapo ukurasa huo upo na utaratibu wa kimtandao unaotumika kuupata ukurasa hiyo.

Mfano wa URL ni:

 • http://jeemu.co.tz/
 • https://developers.google.com/speed/docs/insights/LeverageBrowserCaching
 • http://www.mwananchi.co.tz/Picha/-/1597602/1596066/-/jf2yt6z/-/index.html

Muundo

Domain name ina sehemu kadhaa, zile za kulia zikiwa ni za kiujumla na za kushoto zikiwa ni za kipekee. Ni kama jina lako kamili, jina la ukoo (sehemu ya kiujumla) kulia na lako binafsi (sehemu ya kipekee) kushoto . Sehemu hizi huitwa domains na hutenganishwa na nukta(.).

 • TLD (Top Level Domain) ni ile iliyo kulia zaidi mwa domain name. Kutoka kwenye mifano yetu hapo juu, .net, .com, na .tz zote ni TLD.
 • Middle Level domain huwa zipo katikati mfano, .co na .ac
 • Machine level domain (machine name) huwa kushoto zaidi mfano, google., fanyaict., ifm., maxima.

TLD na middle level domain mara nyingi huwa zina maana na ni kwa matumizi maalum. Mfano:

 • .gov, .go – Taasisi za serikali(gov, go ni kifupisho cha government-serikali)
 • .edu, .ac – Taasisi za elimu (edu ni kifupisho cha education – elimu/ac ni kifupisho cha academic – taaluma)
 • .org, .or – Taasisi za kujitolea (org, or ni kifupisho cha organization)
 • .com, .co – Taasisi za kibiashara (com, co ni kifupisho cha commerce – biashara)
 • .net – Taasisi zinazojihusisha na mambo ya mtandao (net ni kifupisho cha Network – mtandao)
 • .tz, .uk, .ke, n.k – Vifupisho vya nchi husika; kwa mpangilio, Tanzania, UK(Uingereza), Kenya, n.k.
 • Orodha inaendelea na kuendelea kwa kuwa kila baada ya muda fulani vinaanzishwa vifupisho vipya.

Kifuatacho ni nini?

Bila shaka maswali yaliyobaki ni: Kwa nini unahitaji domain name? Ni jinsi gani unaweza kuchagua domain name? Na namna gani unaweza kuisajili?

Kwa leo acha tuishie hapa. Katika post ijayo tutajibu maswali hayo.

Je, wewe ulikuwa unaelewa nini ulipokuwa ukisikia maneno ‘domain name’? Na kipi unahisi wengine wanapaswa kukijua juu ya domain name ingawa sikukigusia katika post hii? Tushirikishe katika comments hapo chini.